Popular Posts

Iran yazindua utaratibu mpya wa kudhibiti meli zinazopita Mlango Bahari wa Hormuz

Iran imezindua rasmi mfumo mpya wa udhibiti wa usafiri wa majini katika Mlango Bahari wa Hormuz.

Press TV imebaini kuwa, kwa mujibu wa utaratibu huo mpya, meli zote zinazokusudia kupita katika Mlango‑Bahari huo zitapokea barua pepe kutoka anwani rasmi ambayo ni info@PGSA.ir ikieleza kwa kina kanuni na taratibu za kuvuka eneo hilo.

Meli zinatakiwa kurekebisha uendeshaji wao kwa mujibu wa mfumo huu na kupata kibali cha kabla ya kuvuka Mlango‑Bahari wa Hormuz, ambao ni miongoni mwa njia muhimu zaidi duniani za kusafirisha mafuta.

Hatua hii, ambayo imeelezwa kama mfumo wa utawala wa kimamlaka , sasa inatumika kikamilifu katika Mlango‑Bahari wa Hormuz, eneo linalokadiriwa kupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayouzwa katika soko la kimataifa.

Vikosi vya ulinzi vya Iran vimeuweka Mlango‑Bahari wa Hormuz chini ya udhibiti mkali, kwa kuzuia meli zote zinazoonekana kuwa na uhusiano na Marekani au Israel, kufuatia vita vya kichokozi vilivyoanzisha na tawala hizo mbili hasimu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu tarehe 28 Februari.

Tehran awali ilionyesha nia ya kurejesha ufunguzi wa Mlango‑Bahari huo baada ya Marekani na Israel kukubali kujumuisha Lebanon katika makubaliano ya kusitisha mashambulizi yaliyosimamiwa na Pakistan, ambayo yalisaidia kusimamisha vita vya siku 40 dhidi ya Iran.

Hata hivyo, Iran zilitangaza tena kufungwa kwa njia hiyo ya maji baada ya Marekani na Israel kutoheshimu masharti ya kusitisha vita.

Muswada wa sheria unaoendelea kujadiliwa katika Bunge la Iran unalenga kupiga marufuku kabisa meli zozote zinazohusishwa na Marekani au Israel kupita Mlango‑Bahari wa Hormuz.

Sheria hiyo pia inaweka msingi wa mfumo wa tozo kwa meli za nchi “zisizo hasimu,” yaani zile ambazo hazihesabiwi kuwa na uadui kwa Iran.

Taharuki imeongezeka kwa kasi katika siku za hivi karibuni baada ya Marekani kuzindua operesheni Jumapili iliyodaiwa kulenga kuvunja udhibiti wa Iran katika Mlango‑Bahari wa Hormuz.

Vikosi vya Iran vimekuwa vikitoa maonyo ya mara kwa mara dhidi ya meli za kivita za Marekani zinazokaribia eneo hilo nyeti.

Siku ya Jumatatu, jeshi la majini la Iran lilirusha makombora na ndege zisizo na rubani (drones) karibu na meli za kivita za  Marekani kwa lengo la kutoa onyo tu. Onyo hilo la kivitendo limetolewa baada ya manoari hizo za Marekani  kupuuzilia mbali miito ya mara kadhaa ya kuacha kukaribia Mlango‑Bahari wa Hormuz.

Maafisa wa Iran wamesisitiza kuwa wataendeleza usimamizi kamili juu ya njia hiyo nyeti ya baharini, wakionya kwamba jaribio lolote la kukabiliana na usimamizi huo wa kisheria litajibiwa kwa nguvu.

 

 

CHANZO: PARS TODAY