Popular Posts

Papa Leo XIV alaani mzunguko wa machafuko Cameroon

Papa Leo wa kumi na nne amelaani kile alichokiita mzunguko usioisha wa machafuko na vifo wakati wa ziara yake katika eneo la Cameroon lililogubikwa na migogoro.

Akiwahutubia waumini katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, papa huyo mzaliwa wa Marekani alisema kuwa waporaji wa rasilimali za nchi hiyo hutumia faida kununua silaha, hivyo kuendeleza machafuko.

Akiwasili chini ya ulinzi mkali, alibariki umati ulioimba na kupeperusha bendera za Vatican na Cameroon. Maeneo mawili yanayozungumza Kiingereza nchini humo yamekumbwa na vita kwa karibu muongo mmoja, baada ya maandamano ya amani kukandamizwa mwaka 2016.

“Wababe wa vita wanajifanya kutojua kwamba inachukua muda mfupi tu kuharibu, ilhali mara nyingi maisha yote hayatoshi kujenga upya. Wanapuuza ukweli kwamba mabilioni ya dola yanatumika kwa mauaji na uharibifu, lakini rasilimali za kuponya, kuelimisha na kurejesha hazipatikani popote.”

Katika hotuba yake, Papa Leo amekemea wanaotumia dini kwa maslahi ya kisiasa na kijeshi. Wafungwa wa kundi la wanaotaka kujitenga wametoa wito kupitia wakili wao kufanyika mazungumzo chini ya usimamizi wa Vatican na ushiriki wa Umoja wa Mataifa.